KOCHA Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi amebainisha kuwa mchezo wao dhidi ya Coastal Union hautakuwa mwepesi lakini wamefanya maandalizi mazuri ili kupata pointi tatu muhimu baada ya dakika 90 za mchezo.
Ni Aprili 7 2025 Yanga wanatarajiwa kumenyana na Coastal Union ya Tanga, saa 10:00 Uwanja wa KMC, Complex ikiwa ni mzunguko wa pili baada ya ule wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Oktoba 26 2024 ubao kusoma Coastal Union 0-1 Yanga.
Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza bao pekee la ushindi kwenye mchezo huo lilipachikwa na mshambuliaji Jean Baleke dakika ya 24 kwa mguu wa kulia akiwa ndani ya 18 likadumu mpaka mwisho wa mchezo na Yanga ikakomba pointi tatu mazima.
Hamdi ameweka wazi kuwa wanatambua ni mchezo muhimu kwao kupata pointi tatu hivyo maandalizi yaliyofanyika yanawapa nguvu kupata matokeo mazuri.
“Tumejiandaa vizuri kuelekea mchezo wetu dhidi ya Coastal Union. Tulikuwa na mchezo mzuri dhidi ya Tabora United na tunaamini tutakuwa na mchezo mzuri dhidi ya Coastal Union, maana mchezo wetu hautakuwa mchezo rahisi na tunakwenda kucheza kwa umakini ili kuhakikisha tunaondoka na alama tatu muhimu,”.
Yanga kwenye msimamo ni namba moja ikiwa na pointi 61 baada yakucheza mechi 23 inakutana na Coastal Union iliyo nafasi ya 13 ikiwa na pointi 25 baada yakucheza mechi 24 msimu wa 2024/25.
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu usipange kukosa.