WAKULIMA wa alizeti, Singida Black Stars wamewabana mbavu mataji wa Dar kwenye mchezo wa ligi mzunguko wa pili kwa kukomba pointi tatu mazima dhidi ya Azam FC katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Liti, Aprili 6 2025 ambapo matajiri Azam FC walisepa wakiwa wameyeyusha pointi tatu mazima.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa dakika 45 za mwanzo ngoma ilikuwa nzito kwa timu zote zilizo ndani ya tano bora hakuna aliyepata Bahati ya kuwanyanyua mashabiki wake jukwaani.
Iliwachukua dakika 75 Singida Black Stars kupata bao la ushindi likifungwa na Elvis Rupia ambaye anafikisha mabao 10 kibindoni akiwa mtupiaji namba moja ndani ya kikosi hicho cha wakulima wa alizeti na alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa mchezo.
Hussen Masanza, Ofisa Habari wa Singida Black Stars ameweka wazi kuwa walikuwa na nafasi kuwafunga mabao zaidi ya matatu kwenye mchezo huo kutokana na kasi waliyokuwa nayo mwanzo mwisho.
“Tumewafunga bao moja ambalo linakera kweli ukiliangalia ila walipaswa kufungwa mabao zaidi ya matatu kwa kuwa wachezaji walitengeneza nafasi nyingi ambazo hazikutumika kwenye mchezo kuwa bao.
“Muhimu tumeshinda mchezo wetu haukuwa mwepesi, tunawapongeza wachezaji kwa kujituma na mwisho kupata ushindi, kazi bado inaendelea na ushindani ni mkubwa.”
Singida Black Stars kwenye msimamo ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 50 nafasi ya tatu ni Azam FC yenye pointi 51 zote zimecheza mechi 25.
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu usipange kukosa.