SIMBA WANATAKA KUPATA BAO UGENINI KIMATAIFA

BENCHI la ufundi la Simba chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids, limeweka wazi kuwa mpango mkubwa kwenye mchezo wa ugenini hatua ya Kombe la Shirikisho Afrika robo fainali ni kuona kwamba wanapata bao ugenini.

Huu ni mchezo wa mtoano ambapo kete ya kwanza Simba watakuwa ugenini na kete ya pili watakuwa Uwanja wa Mkapa, Aprili 9 kwenye msako wa mshindi wa jumla katika mchezo huo wa dakika 180.

Machi 28 2025 kikosi cha Simba kilitua Misri na kufanya maandalizi kwa muda wa siku nne ambapo Fadlu ameweka wazi kuwa yalikuwa maandalizi mazuri tayari kwa mchezo dhidi ya wapinzani wao Al Masry Uwanja wa Suez.

Ni Che Malone ambaye ni beki, Aishi Manula kipa, Valentino Mashaka ambaye ni mshambuliaji na Mzamiru Yassin kiungo hawapo kwenye mpango wa mchezo wa leo kutokana na kutokuwa fiti.

Moussa Camara, kipa namba moja wa Simba kuanza kwake kutategemea ripoti ya madaktari kwa kuwa alipata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Azam FC bado hakuwa fiti kwa asilimia 100.

Fadlu amesema: “Tunachohitaji kwenye mchezo wetu ugenini ni kuona kwamba tunapata bao kwa kuwa tuna kazi kwenye mchezo ujao Uwanja wa Mkapa ambao tunaamini kwamba huko tutapambana kupata matokeo chanya, mchezo utakuwa mgumu lakini tupo tayari.”

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu usipange kukosa.