SILAHA ILIYOWAANGAMIZA SIMBA KARIAKOO DABI YAFUNGUKA

NYOTA wa Yanga Princess, Jeannine Mukandayisenga muuaji wa Simba Queens kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi uliochezwa Uwanja wa KMC Complex amefichua siri kuwa walipewa maelekezo na benchi la ufundi lialoongozwa na Edna Lema namna ya kuuvunja ukuta wa Simba.

Ushindi wa Yanga Princess unavunja rekodi ya kukwama kupata pointi tatu kwenye mechi tanoambazo ni dakika 450 walipokutana uwanjani kwenye mechi za hivi karibuni.

Rekodi zinaonyesha kuwa kwenye mechi hizo tano, ushindi kwa Simba Queens ilikuwa katika mechi tatu, waligawana pointi mojamoja kwenye mechi mbili huku yakifungwa jumla ya mabao 13 ndani ya uwanja.

Katika mabao hayo, Simba Queens ilifunga jumla ya mabao 9 na Yanga Princess ikifunga mabao 5, rekodi hiyo imetibuliwa kwenye mchezo wa sita ambapo Yanga Princess ilipata pointi tatu mazima ndani ya dakika 90.

Hivyo kwenye mechi sita, Yanga imepata ushindi mara moja na kugawana pointi mojamoja mara mbili huku ikipoteza mara tatu kwenye Ligi ya Wanawake Tanzania.

Jeannine amesema kuwa walipata maelekezo kutoka kwa benchi la ufundi na kuyatumia kwa umakini kwenye kutafuta ushindi jambo ambalo ni furaha kwao kuvuna pointi tatu kwenye mechi kubwa.

“Mwalimu alituambia kwamba lazima tuwakabili mabeki wa Simba bila kuongopa ili kupata ushindi, tulikubaliana kufanya hivyo na tukapata ushindi hili kwetu ni kubwa na tumefurahi kwa kuwa tulikuwa tunahitaji pointi tatu.”

Edna Lema, Kocha wa Yanga Princess amesema kuwa maelekezo yake yalitumiwa vizuri na wachezaji jambo ambalo limewapa ushindi kwenye mchezo huo.

“Ni furaha kuona kwamba tumepata ushindi ninawapongeza wachezaji kwa kufuata maelekezo kwenye mchezo wetu ambao ulikuwa mgumu, mashabiki kujitokeza na namna ambavyo viongozi wapo pamoja nasi.”

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu usipange kukosa.