KIBU AFUNGUKIA TUZO YAKE BONGO

KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Kibu Dennis maarufu kwa jina la mkandaji amechekelea kutwaa tuzo yake ya kwanza ndani ya Ligi Kuu Bara namba nne kwa ubora Afrika baada ya kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo dhidi ya Dodoma Jiji, Uwanja wa KMC Complex.

Ikumbukwe kwamba Machi 14 2025 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa KMC Complex ulisoma Simba 6-0 Dodoma Jiji ukiwa ni ushindi wa pili mkubwa kwa Simba kupata msimu wa 2024/25 ule wa kwanza ilikuwa Kagera Sugar 2-5 Simba.

Katika mchezo huo Kibu alihusika kwenye mabao manne, alifunga mabao mawili na kutoa pasi mbili za mabao akachaguliwa kuwa mchezaji bora kwenye mchezo huo walipokomba pointi tatu mazima Simba.

Ni mara ya kwanza Kibu anatwaa tuzo hiyo kwenye ligi huku akifungua akaunti ya mabao ndani ya ligi kwa kuwa mara ya mwisho kufunga ilikuwa ni Novemba 5 2023 katika mchezo wa Kariakoo Dabi uliochezwa Uwanja wa Mkapa.

Kibu amesema kuwa walikuwa wanahitaji ushindi kwenye mchezo huo na walianza kwa kasi baada ya kupokelewa vizuri na mashabiki jambo ambalo liliwapa nguvu kupambana zaidi.

“Ilikuwa ni mwanzo mzuri hasa ukizingatia kwamba mashabiki walitupokea vizuri na mwisho tukapata ushindi hii ni furaha kwetu. Nimefurahi kupata tuzo kwa kuwa sio kitu chepesi hasa ukizingatia kuna wachezaji zaidi ya 20 walikuwa uwanjani.”

Safu ya ushambuliaji ya Simba ndani ya ligi ni namba mbili kwa kutupia mabao mengi ambayo ni 52 vinara wakucheka na nyavu ni Yanga ambao safu yao ya ushambuliaji imetupia jumla ya mabao 58 baada ya mechi 22 huku Simba ikiwa imecheza mechi 21.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM.