MAKIPA YANGA NA SIMBA KWENYE VITA YAO HUKO

KUNA kazi nzito ndani ya uwanja kwenye msako wa pointi tatu muhimu kwa wababe wawili ambapo kila kona kuna kisanga cha maana kutokana na ubora wa Ligi Kuu Bara inayodhaminiwa na NBC ikiwa ni namba nne kwa ubora Afrika.

Weka kando vita ya kusaka ushindi ndani ya uwanja kwenye Kariakoo Dabi mchezo unaotarajiwa kuchezwa Machi 8 2025 Uwanja wa Mkapa kuna beto nyingine upande wa makipa nani ambaye atasepa na hati safi na mwamuzi atakuwa ni Ahmed Arajiga kutoka Manyara..

Ikumbukwe kwamba kwenye vita ya mwanzo ni Djigui Diarra aliibuka shujaa kwa kusepa na dakika 90 bila lango lake kutikiswa ambapo ubao ulisoma Simba 0-1 Yanga, Moussa Camara wa Simba aliokota bao nyavuni baada ya beki Kelvin Kijili kujifunga kwenye mchezo huu mwamuzi alikuwa ni Ramadhan Kayoko.

Ni Diarra yeye kakaa langoni kwenye mechi 16 msimu wa 2024/25 ndani ya kikosi cha Yanga akiwa kakomba dakika 1451 katika dakika hizo akiwa uwanjani katunguliwa jumla ya mabao 7 na mchezo ambao aliruhusu mabao mengi ilikuwa Yanga 1-3 Tabora United.

Kwenye mechi hizo 16 kakusanya hati safi 11 hivyo ni mechi tano pekee Diarra alikwama kukusanya hati safi ndai ya uwanja kwenye mechi za ushindani katika ligi namba nne kwa ubora Afrika.

Diarra ana wastani wakuokota bao moja kila baada ya dakika 207, alianza kikosi cha kwanza mchezo uliopita dhidi ya Pamba Jiji aliposhuhudia ubao ukisoma Pamba Jiji 0-3 Yanga, mabao mawili yalifungwa na Aziz Ki na bao moja lilifungwa na Chadrack Boka.

Kwa upande wa Camara ambaye ni kipa namba moja wa Simba ni mechi 20 alianza kikosi cha kwanza kati ya 21 ambazo timu hiyo imecheza kwa msimu wa 2024/25. Katunguliwa mabao 8 miongoni mwa hayo alifungwa kwenye Kariakoo Dabi.

Camara amekusanya jumla ya hati safi 15 akiwa katunguliwa kwenye mechi tano kati ya 20 ambazo alianza langoni kutimiza majukumu yake. Ana wastani wakufungwa bao moja kila baada ya dakika 225 akiwa langoni. Mechi tatu aliruhusu mabao mawili ilikuwa dhidi ya Kagera Sugar, Azam FC na Coastal Union.

Kipa huyo hakuanza kikosi cha kwanza mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union ambapo alishuhudia langoni akianza Ally Salim na mwisho ubao ukasoma Coastal Union 0-3 Simba. Kazi inatarajiwa kupigwa Machi 8 kujua nani atakuwa shujaa baada ya dakika 90.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM.