SIMBA WAPOTEANA KWA MKAPA, KOCHA AKASIRISHWA NA MATOKEO

REKODI ya kipa namba moja wa Simba, Mousa Camara kuvuna hati safi mbele ya Azam FC kwa mara nyingine tena mzunguko wa pili, Februari 24 2025 iligonga mwamba kwa kushuhudia akitunguliwa mabao mawili ndani ya dakika 90.

Mapema Camara alitunguliwa dakika ya kwanza na nyota wa Azam FC, Gibrill Sillah na bao hilo liliwekwa usawa na Ellie Mpanzu dakika ya 25 na kuweka usawa mpaka dakika 45 za mwanzo.

Kipindi cha pili ni beki Hamza Jr alipachika bao la pili kwa Simba likiwa ni bao lake la kwanza ndani ya msimu akitumia pasi ya Jean Ahoua ambaye alipiga faulo dakika ya 76 kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Simba wakiwa wanaamini mchezo umegota mwisho watasepa na pointi tatu wakapoteana baada ya bao la Zidane Sereri dakika ya 88 akitumia pasi ya maelekezo kutoka kwenye miguu ya Feisal Salum ikiwa ni pasi yake ya 11 ndani ya msimu  akiwa mkali namba moja kwa vinara wa pasi za mwisho ndani ya ligi namba nne kwa ubora.

Kwenye msimamo Simba ni namba mbili akiwa na pointi 51 baada ya mechi 20 huku Azam FC ikiwa nafasi ya tatu na pointi 44 baada ya mechi 21 vinara wakiwa ni Yanga wenye pointi 55 baada ya mechi 21.

Fadlu Davids, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa hawajafurahia matokeo hayo kwa kuwa walikuwa wanapambana kusaka pointi tatu makosa ambayo walifanya yamewaadhibu huku akipongeza kiwango cha wapinzani wao Azam FC.

“Hatujafurahishwa na matokeo kutokana na maandalizi yetu na mahitaji ya pointi tatu muhimu, tulipata bao la kuongoza kipindi cha pili na mwisho tumegawana pointi mojamoja haya ni matokeo ambayo hatujayapenda hivyo tunakwenda kufanyia kazi makosa ili kuwa bora kwa mechi zijazo.”

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM.