KADI NYEKUNDU YA DERICK MUKOMBOZI DHIDI YA SIMBA YAFUTWA

KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imefuta adhabu ya kadi nyekundu (Red Card) aliyooneshwa mchezaji wa Namungo, Derick Mukombozi na mwamuzi wa mchezo wa Ligi Kuu ya NBC kati ya Namungo dhidi ya Simba Sc.

Taarifa ya leo Februari 23, 2025 iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya mapitio ya mwenendo na matukio ya Ligi katika kikao chake cha Februari 21, 2025.

Kamati imefikia maamuzi hayo baada ya kujiridhisha kuwa maelezo yaliyopo kwenye ripoti ya mwamuzi hayana ushahidi wa kutosha unaoendana na marejeo ya picha mjongeo kuwa Mukombozi alistahili kadi nyekundu.