PAMBA JIJI KUMBE SIO WEPESI HUKO

WAKULIMA wa Pamba kutoka Jiji lenye madini ya mawe, Mwanza, Pamba Jiji wamedhihirisha kuwa sio wepesi kama ilivyo Pamba kutokana na kupata matokeo mbele ya matajiri wa Dar kwenye mchezo wa ligi inayodhaminiwa na NBC.

Ikiwa ni ligi namba nne kwa ubora ushindani wake umezidi kuwa mkubwa hasa mzunguko wa pili ambapo vigogo wamekuwa wakiangusha pointi kwenye mechi zao za ushindani.

Matajiri wa Dar, Azam FC mbele ya Pamba Jiji kwenye mchezo wa ligi waliyeyusha pointi tatu mazima ugenini katika msako wa pointi tatu muhimu ndani ya dakika 90.

Katika mchezo huo uliochezwa Februari 9 2025 ngoma ilikuwa nzito kwa timu zote mpaka dakika ya 86 kwa bao la kiungo mshambuliaji Deus Kaseke ambaye alipachika bao hilo la ushindi lililodumu mpaka mwisho wa mchezo.

Azam FC inabaki na pointi 39 kwenye msimamo ni namba tatu huku Pamba Jiji ikifikisha pointi 18 nafasi ya 12 kwenye msimamo, ina wastani wa kukomba pointi moja kwenye kila mchezo kwa kuwa ni mechi 18 imecheza ndani ya msimu wa 2024/25.

Vinara wa ligi ni Yanga wenye pointi 45 baada ya kucheza mechi 17 na safu yao ya ushambuliaji imetupia jumla ya mabao 42 ikiwa ni timu namba moja kufunga mabao mengi kwenye ligi.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM.