MATAJIRI wa Dar, Azam FC wamemalizana na KMC ndani ya msimu wa 2024/25 kwa kukomba pointi zote sita mazima.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Azam FC walipata ushindi wa mabao 4-0 Uwanja wa KMC Complex na bao la kwanza ndani ya Azam FC kwenye ligi likifungwa na Idd Nado akitumia pasi ya Fei Toto.
Hiyo ilikuwa ni Septemba19 2024 Azam FC walipopata ushindi wa kwanza ndani ya ligi wakiwa ugenini na Fei alichaguliwa kuwa mchezaji bora.
Kwenye mchezo wa mzunguko wa pili uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Februari 6 2025 ubao ulisoma Azam FC 2-0 KMC.
Mabao ya Azam FC yalifungwa na Gibril Sillah dakika ya 27 na 66 kwa pasi ya Fei Toto ambaye anafikisha pasi 10 za mabao ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ni ligi namba nne kwa ubora.
Azam FC inafikisha pointi 39 nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi vinara wa ligi ni Yanga wenye pointi 45 baada ya mechi 17. Mchezo ujao kwa Azam FC itakuwa dhidi ya Pamba Jiji, Februari 9 2025.