Home Sports GAMONDI AZIPIGIA HESABU KALI POINTI ZA SIMBA

GAMONDI AZIPIGIA HESABU KALI POINTI ZA SIMBA

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi raia wa Argentina, amefichua kwamba, ana kazi kubwa mbele ya kuhakikisha anapata matokeo mazuri katika michezo yake mitatu ijayo ikiwemo dhidi ya Simba kabla ya kugeukia michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa lengo la kupunguza presha ya kupambania ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Gamondi ametoa kauli ikiwa Yanga ina michezo mitatu ambayo ni sawa na dakika 270 ikicheza dhidi ya Singida Fountain Gate (Oktoba 26), Simba (Novemba 5) na Coastal Union (Novemba 8), kisha watageukia Ligi ya Mabingwa Afrika kupambana na CR Belouizdad ya Algeria kati ya Novemba 24 na 25.

Kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Azam, Yanga ilikuwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 12, wakati Azam ikiwa nafasi ya pili na pointi zao 13. Vinara walikuwa Simba wenye pointi 15.

Akizungumza na Spoti Xtra, Gamondi alisema moja ya jukumu kubwa ambalo lipo mbele yake ni kuhakikisha wanafanya vizuri katika michezo hiyo kwa kuwa wanataka kupunguza presha kubwa iliyopo kwao baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Ihefu katika Ligi Kuu Bara.

“Tumepoteza mchezo ambao hatukutarajia, kwa sasa tunajaribu kuweka malengo katika michezo ambayo ipo mbele yetu kwa sababu ya kupunguza pengo la pointi na kubaki kwenye kile ambacho tunatarajia kukifanya msimu huu.

“Ukweli ni kwamba, ligi ni ngumu, lakini hatuwezi kusema tunataka kurudi nyuma kwa sababu hizi mechi ambazo zipo mbele yetu zinahitaji kupata matokeo mazuri kabla ya kuanza kuangalia michuano ya kimataifa.

“Nataka kuona timu inashinda hizi mechi kabla ya kuangalia Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sababu dhamira ya kutetea ubingwa wetu msimu huu haiwezi kupotea,” alisema Gamondi.

Previous articleHAPA NDIPO TATIZO LA SIMBA KUONDOLEWA NA AL AHLY
Next articleVIDEO: SIMBA TUMEKUFA KIUME/ DUA ZILIKUWA MPIRA UISHE