Home Sports MUSONDA AWATIBULIA MASTAA YANGA

MUSONDA AWATIBULIA MASTAA YANGA

MFUMO wa 4-4-2 anaotumia Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi kwa kuwachezesha washambuliaji wawili, huenda ukawavurugia viungo wa timu hiyo baadhi kujikuta wakisotea benchi katika michezo ijayo.

Hiyo ni baada ya Yanga kufanikiwa kuipata saini ya mshambuliaji Mzambia, Kennedy Musonda katika usajili wa dirisha dogo uliofungwa Januari 15, mwaka huu.

Nabi amelazimika kutumia mfumo wa 4-4-2 akiwatumia washambuliaji wawili, Fiston Mayele na Kennedy Musonda katika mchezo wa Ligi kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting, uliochezwa Jumatatu ya wiki hii.

Katika mchezo huo, washambuliaji hao ilikuwa mara ya kwanza kucheza pamoja dakika zote tisini, baada ya awali Musonda kutokea benchi dhidi ya Ihefu.

Wakati kabla ya kutua Musonda, kocha huyo alikuwa akitumia mfumo wa 4-2-3-1, akitumia viungo wa kati watatu na mawinga wawili, huku mshambuliaji akiwa mmoja ambaye ni Mayele. Mfumo huo mpya utamlazimu Nabi kutumia viungo wawili wa kati badala ya watatu.

Nabi alianza kuutumia mfumo huo katika mchezo wa ligi dhidi ya Ihefu FC uliochezwa Uwanja wa Mkapa baada ya Musonda kuingia, kisha akaendelea dhidi ya Ruvu. Mechi zote Yanga ilishinda 1-0.

Akizungumzia hilo, Nabi alisema: “Katika mechi hizi mbili tumekuwa tukijaribu kuingiza mfumo mpya wa kucheza na washambuliaji wawili ndio maana imekuwa ikileta changamoto kidogo ya ufungaji.

“Tutarejea kwenye viwanja vya mazoezi kuboresha, lakini pia kuna baadhi ya wachezaji walikosekana, Fei Toto (Feisal Salum), Aucho (Khalid), Morrison (Bernard), Aziz Ki (Stephane) na Bangala (Yannick).

“Tunaamini kwenye michezo ijayo baadhi yao watarejea, lakini kitu kikubwa zaidi kwetu kuliko vyote tunavyozingatia ni kupata pointi tatu.”

Previous articleNABI AWEKA REKODI MPYA YANGA
Next articleHAALAND MOTO CHINI, KAZI NYINGINE LEO USIKU