Home Sports YANGA WATAMBA WANAPIGA POPOTE

YANGA WATAMBA WANAPIGA POPOTE

HUKU wengi wakiamini Yanga SC kuanzia nyumbani katika mchezo wa hatua ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal itawazuia kufuzu hatua ya makundi, kocha msaidizi wa timu hiyo, Cedric Kaze ameibuka na kushusha presha kwa kusema kikosi chao kinaweza kupata ushindi popote.

Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, wamefuzu hatua ya Pili Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuwaondosha Zalan FC ya Sudan Kusini kwa matokeo ya jumla ya mabao 9-0.

Katika hatua ya kwanza, Yanga watavaana na Al Hilal ya Sudan ambapo mchezo wa kwanza utapigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Oktoba 8, mwaka huu.

Kuhusu maandalizi ya kikosi chao, Kaze amesema: “Hatuwezi kusema mchezo wetu uliopita dhidi ya Zalan ulikuwa kipimo sahihi katika mashindano haya, ni kweli tunawaheshimu lakini nadhani kwetu Al Hilal watatupa changamoto nzuri.

“Tumezungumza na wachezaji wetu kuwakumbusha juu ya hilo, kuhakikisha wanasahau matokeo ya michezo iliyopita na kuanza upya, tutaanzia nyumbani katika mchezo huu, lakini kwa ubora wa kikosi tulichonacho tunaamini tunaweza kupata matokeo mazuri popote na kufuzu hatua inayofuata.”

Baada ya mchezo huo wa nyumbani, Yanga itaenda Sudan kurudiana na Al Hilal, mechi ikipangwa kuchezwa kati ya Oktoba 14-16, mwaka huu ambapo mshindi wa jumla atafuzu hatua ya makundi.

Previous articleVIDEO:HUYU HAPA CEO MPYA YANGA, RAIS AMZUNGUMZIA
Next articleSAUTI:KOCHA MBRAZIL AIBUKIA SIMBA