Fountain Gate Academy Tanzania iko katika hatua za kuanzisha chuo cha michezo kitakachojulikana kama Fountain Gate Institute of Sports and Talent Development, ambapo tawi la kwanza linatarajiwa kufunguliwa Babati, Manyara, hivi karibuni.
Kupitia taasisi hii, Fountain Gate Academy inalenga kuimarisha zaidi programu zake za michezo, hususan Football Development, kwa kuhakikisha vijana wanapata mafunzo ya kisasa, yenye viwango vya kimataifa na yanayolenga kukuza vipaji kwa njia ya kitaalamu na endelevu.
Katika kufanikisha azma hiyo, Rais wa Fountain Gate Academy Japhet Makau yupo nchini Hispania katika hatua za mwisho za kukamilisha makubaliano ya kutumia mitaala ya Marcet Football University, taasisi inayotambulika kimataifa kwa mfumo wake wa kitaalamu wa maendeleo ya wachezaji na programu za soka.
Hivyo, safari hii inalenga kukamilisha majadiliano na taratibu za ushirikiano kati ya Fountain Gate Academy na Marcet Football University, pamoja na kukamilisha na kusaini Memorandum of Understanding (MoU) itakayoweka msingi rasmi wa ushirikiano huo.
Ushirikiano huu unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa Fountain Gate wa kutambua, kulea na kuendeleza vipaji vya vijana, huku ukiwaunganisha na mfumo wa mafunzo wenye viwango vya kimataifa.