KIPRE JR ATANGAZWA KLABU YA MOULOUDIA YA ALGERIA

KLABU ya Mouloudia Algiers ya Algeria imekamilisha usajili wa aliyekuwa winga wa Azam FC, Kipré Zunon Junior kwa mkataba wa miaka minne utakaombakisha klabuni hapo mpaka 2028.

Azam FC itapokea kitita cha dola 300,000 (takribani milioni 797) kwa mauzo ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 raia wa Ivory Coast.

Matajiri wa Dar Azam FC hawakuwa kwenye mpango wa kumuuza nyota huyo lakini Waarabu hao kutoka Algeria walibisha hodi kwenye viunga vya Azam FC.

Anaingia kwenye orodha ya nyota waliokuwa wakipigiwa hesabu na timu kubwa Bongo zikapishana naye kutona na dau ambalo lilikuwa linahitajika na mabosi hao wa Azam FC.

Alikuwa ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu Yusuph Dabo kutokana na uwezo wake kwenye umiliki wa mpira pamoja na pasi za maelekezo kwa wachezaji wa Azam FC.